Sera za Mpango wa Gmail

Sera za Mpango zilizo hapo chini zinatumika katika Gmail. Sera hizi zina nafasi muhimu katika kudumisha hali nzuri kwa ajili ya kila mtu anayetumia Gmail.

Ikiwa unatumia Gmail kwa akaunti ya mtumiaji (k.m., @gmail.com), tafadhali pia rejelea Sheria na Masharti ya Google ili upate maelezo zaidi. Ikiwa unatumia akaunti kupitia kazi, shule au shirika lingine, masharti yanaweza kutumika kulingana na makubaliano ya shirika lako na Google au sera zingine. Msimamizi wako anaweza kutoa maelezo zaidi.

Tunahitaji kuzuia matumizi mabaya yanayotishia uwezo wetu wa kutoa huduma hizi na tunaomba kila mtu atii sera zilizo hapo chini ili kutusaidia kufanikisha lengo hili. Baada ya kuarifiwa kuhusu jambo ambalo huenda linakiuka sera zetu, tunaweza kukagua maudhui hayo na kuchukua hatua, ikiwa ni pamoja na kumwekea mtumiaji mipaka au kuondoa idhini yake ya kufikia bidhaa za Google. Ikiwa akaunti yako imefungwa na unaamini kuwa ilifungwa kimakosa, tafadhali fuata maagizo yaliyo kwenye ukurasa huu.

Tunaweza kuchukua hatua dhidi ya akaunti zinazotumia nafasi inayozidi vikomo vilivyowekwa vya nafasi ya hifadhi. Kwa mfano, tunaweza kuzuia kutuma au kupokea barua pepe ikiwa umezidi kikomo chako cha nafasi ya hifadhi. Tunaweza pia kufuta maudhui kwenye akaunti yako ukikosa kupunguza nafasi ya hifadhi unayotumia au usipoongeza nafasi ya ziada ya kutosha. Soma maelezo zaidi kuhusu vikomo vya nafasi ya hifadhi hapa.

Tafadhali zirejelee mara kwa mara kwa sababu sera hizi zinaweza kubadilika.

Ripoti matumizi mabaya

Ikiwa unaamini kwamba akaunti fulani imekiuka Sera zetu za Mpango, kuna njia nyingi za kuiripoti:

  • Kwa matumizi mabaya ya kawaida, tumia fomu hii
  • Kwa vitendo vya kupevua watoto, tumia fomu hii
  • Kwa ukiukaji wa hakimiliki, tumia fomu hii

Hakikisha umesoma sera zilizo hapo chini ili uelewe jinsi tunavyofafanua matumizi mabaya. Google inaweza kufunga akaunti zinazopatikana kuwa zinakiuka sera zetu. Ikiwa akaunti yako imefungwa na unaamini ilifungwa kimakosa, tafadhali fuata maelekezo yaliyo kwenye ukurasa huu.

Akaunti Kutotumika

Tumia bidhaa ili akaunti yako iwe inatumika. Kutumia bidhaa inamaanisha kufikia bidhaa au maudhui yake angalau kila miaka miwili. Tunaweza kuchukua hatua dhidi ya akaunti ambazo hazitumiki, ikiwa ni pamoja na kufuta barua pepe zako kwenye bidhaa. Soma maelezo zaidi hapa.

Barua Pepe Taka na Zile Zinazotumwa kwa Wapokeaji Wengi

Usitumie Gmail kusambaza barua taka au barua pepe za biashara ambazo hazijaitishwa na wapokeaji.

Huruhusiwi kutumia Gmail kutuma barua pepe zinazokiuka Sheria ya CAN-SPAM au sheria zingine dhidi ya barua taka; kutuma barua pepe ambazo hazijaidhinishwa kupitia seva za wahusika wengine, au zilizo wazi; au kusambaza anwani ya barua pepe ya mtu yeyote bila idhini yake.

Huruhusiwi kufanya kiolesura cha Gmail kiweze kufanya yafuatayo kiotomatiki; kutuma, kufuta, au kuchuja barua pepe, kwa namna inayopotosha au kuwahadaa watumiaji.

Tafadhali kumbuka kwamba unachokiita barua pepe “zisizoitishwa” au “zisizotakikana” kinaweza kuwa tofauti na mtazamo wa anayepokea barua pepe zako. Tumia busara unapotuma barua pepe kwa idadi kubwa ya wapokeaji, hata kama wapokeaji hao walichagua kupokea barua pepe kutoka kwako hapo awali. Watumiaji wa Gmail wanapotia barua pepe alama kuonyesha ni barua taka, hili huongeza uwezekano kwamba barua pepe utakazotuma hapo baadaye pia zitachukuliwa kuwa ni barua taka na mifumo yetu inayolinda dhidi ya matumizi mabaya.

Kufungua na Kutumia Akaunti Nyingi za Gmail

Usifungue wala usitumie akaunti nyingi kukiuka sera za Google, kukwepa vizuizi vya akaunti za Gmail, kuepuka vichujio au kubatilisha kwa njia nyingine mipaka iliyowekwa kwenye akaunti yako. (Kwa mfano, kama umezuiwa na mtumiaji mwingine au akaunti yako ya Gmail imefungwa kwa sababu ya matumizi mabaya, usifungue akaunti nyingine ya kufanya shughuli kama hizo.)

Huruhusiwi pia kufungua akaunti za Gmail kwa njia za kiotomatiki wala huruhusiwi kununua, kuuza, kubadilisha au kuuza tena akaunti za Gmail kwa watu wengine.

Programu Hasidi

Usitumie Gmail kusambaza virusi, programu hasidi, vidudu, hitilafu, programu hasidi za Trojan, faili zilizovurugika au vitu vingine vyovyote vya uharibifu au udanganyifu. Vilevile, usisambaze maudhui yanayodhuru au kukatiza utendakazi wa mitandao, seva au miundo msingi mingine ya Google au ya wengine.

Ulaghai, Wizi wa Data Binafsi na Shughuli Zingine za Udanganyifu

Huruhusiwi kufikia akaunti ya Gmail ya mtumiaji mwingine bila ruhusa yake dhahiri.

Usitumie Gmail kuiba data binafsi. Jiepushe na kuombaomba au kukusanya data nyeti, ikiwa ni pamoja na, lakini si tu manenosiri, maelezo ya kifedha na Nambari za Usalama wa Jamii.

Usitume barua pepe ili kuwadanganya, kuwapotosha au kuwahadaa watumiaji wengine washiriki taarifa kwa hila. Hii inajumuisha kuiga mtu, kampuni au shirika lingine kwa nia ya kuhadaa au kupotosha.

Usalama wa Watoto

Google ina sera ya kupinga vikali maudhui yanayoonyesha unyanyasaji wa ngono dhidi ya watoto. Tukitambua maudhui kama hayo, tutapiga ripoti kwa shirika la National Center for Missing and Exploited Children kama inavyohitajika kisheria. Tunaweza pia kuchukua hatua za kinidhamu, ikiwa ni pamoja na kufunga Akaunti za Gmail za waliohusika.

Google imepiga marufuku vitendo vya kupevua watoto kwa kutumia Gmail. Vitendo hivi vinafafanuliwa kuwa vinavyolenga kujenga uhusiano na mtoto ili kupunguza wasiwasi wake kwa madhumuni ya kumtayarisha kwa unyanyasaji wa kingono, ulanguzi au unyanyasaji mwingine.

Ikiwa unaamini kuwa kuna mtoto aliye hatarini au amedhulumiwa, amenyanyaswa au ni mhasiriwa wa ulanguzi, wasiliana na vitengo vya utekelezaji wa sheria mahali ulipo mara moja.

Ikiwa tayari umeripoti kwa vitengo vya utekelezaji wa sheria na bado unahitaji usaidizi, au una wasiwasi kuwa kuna mtoto anayehatarishwa au aliyehatarishwa kwenye Gmail, unaweza kuripoti tabia hiyo kwa Google ukitumia fomu hii. Tafadhali kumbuka kwamba unaweza kumzuia mtu yeyote ambaye hutaki awasiliane nawe kwenye Gmail.

Hakimiliki

Fuata sheria za hakimiliki. Usikiuke haki za uvumbuzi za watu wengine, zikiwemo hataza, chapa za biashara, siri za biashara au haki zingine za umiliki. Huruhusiwi kuwahimiza au kuwashawishi watu wengine kukiuka haki za uvumbuzi za watu wengine. Unaweza kuripoti ukiuakji wa hakimiliki kwa Google kwa kutumia fomu hii.

Unyanyasaji

Usitumie Gmail kuwanyanyasa, kuwaogofya au kuwatisha watu wengine. Akaunti ya mtu yeyote atakayepatikana akitumia Gmail kwa madhumuni kama haya itafungwa.

Shughuli Haramu

Fuata sheria. Usitumie Gmail kuendeleza, kupanga au kushiriki katika shughuli zilizo kinyume cha sheria.